WATU watano wanahofi wa kufa akiwemo rubani wa helikopta iliyokuwa ikitoka eneo la Jarika Kaunti ya Nakuru kuelekea Tipis, Mau Narok kwenye kampeni za Rais Uhuru Kenyatta, kuanguka katika Ziwa Nakuru
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya (KCAA), Gilbert Kibe, helikopta hiyo ilikuwa na watu watano akiwamo rubani wake Bootsy Mutiso.
“Hadi sasa hakuna tena matumaini ya kupata majeruhi kwa sababu helikopta hiyo imezama kwenye ziwa hili na juhudi za uokozi zinaendelea kwa kuleta boti kutoka Ziwa Naivasha, ila sasa ndege zinapita juu kuangalia iwapo wataona chochote na kusaidia,” alisema Kibe.
Alisema katika ziwa hilo la Nakuru hakukuwa na boti karibu hivyo imebidi boti itoke Naivasha ambako ni mbali na hivyo uwezekano wa kuwapata waathirika wakiwa hai ni mdogo.
Kibe alisema katika helikopta hiyo mbali ya rubani, kulikuwa na wanaume watatu na mwanamke mmoja ambao hata hivyo hadi jana jioni majina yao yalikuwa hayajatambuliwa. Alisema helikopta hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Flex Air Charters.
Awali Seneta wa Nakuru, Susan Kihika alisema abiria watatu kati ya hao wanne ni watumishi wenzake katika kitengo cha mawasiliano. Alisema helikopta hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka Jarika Kaunti na mashuhuda wengine wanasema waliiona ikiruka umbali wa chini kabla ya kuanguka.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kitengo cha Taifa cha Maafa, Pius Masai alisema wametuma helikopta moja ya Polisi kwenda kusaidia uokozi. “Pia tumetuma wazamiaji kutoka Jeshi la Wanamaji la Kenya wasaidie kutafuta helikopta hiyo iliyozama ziwani,”alisema Masai.
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo viongozi mbalimbali walifika kwenye ziwa hilo akiwemo Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui na viongozi wengine wakiwemo wabunge wa eneo hilo.
Wabunge hao ni Samuel Arama ( Nakuru Magharibi), David Gikaria (Nakuru Mashariki), Jayne Kihara (Naivasha) na Liz Chelule (Mwakilishi wa wanawake). Pia alikuwepo Spika wa Kaunti ya Nakuru, John Kairu.
No comments:
Post a Comment